Mshindi wa mashindano ya Mumbai Marathon ambaye ni balozi maalum wa Kampuni ya Multichoice Tanzania, Alphonce Felix Simbu, amewashukuru Watanzania kwa kuendelea kumsapoti na amewaomba kwa pamoja washirikiane kuitangaza nchi kimataifa.
Simbu ameyasema hayo leo kwenye hafla fupi ya kumpongeza iliyoandaliwa na kampuni hiyo iliyofanyika kwenye Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.
Hafla hiyo imekuja baada ya Jumapili ya wiki iliyopita Simba kufanikiwa kushika nafasi ya kwanza kwenye mbio za Mumbai Marathon zilizofanyika India na kuwabwaga Wakenya na Waethiopia walioshika nafasi ya pili mpaka kumi.
“Kama mlifuatilia zile mbio, katika kumi bora, kulikuwa na Wakenya saba na Waethiopia wawili, huku Mtanzania nikiwa peke yangu, kama nisingejitahidi basi Tanzania tusingekuwa na furaha kama hii.
“Hivyo niombe tu tushirikiane wakati mwingine tuandae wanariadha wengi ili kuwa na nafasi kubwa ya kushinda, naamini tukifanya hivyo nchi yetu itakuwa juu ndani ya kipindi kifupi,” alisema Simbu.
Wakati huohuo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, alisema: “Nichukue fursa hii kumpongeza shujaa wetu Simbu na Kampuni ya Multichoice kwa kuitangaza nchi kimataifa, ushindi ulioletwa na Simbu ni mkubwa na umeitangaza Tanzania.
“Serikali peke yake haiwezi kufanikisha hili, hivyo nitoe wito kwa makampuni binafsi kuja kwetu tushirikiane kuwekeza katika vipaji kama hivi, tunataka siku zijazo tuwe na mashujaa wengi kama Simbu, isiwe tu kwenye michezo, bali hata katika muziki na sanaa mbalimbali, naamini dunia itatutambua vilivyo.”
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Multichoice Tanzania, Ronald Baraka Shelukindo, alisema wataendelea kumdhamini Simbu, na wanataka awe chachu na hamasa kwa vijana wanaochipukia ili waone kweli kila kitu kinawezekana, kikubwa ni kujituma tu.
No comments:
Post a Comment