AJTC COLLEGE

Friday, 20 January 2017

MASHABIKI SIMBA, YANGA WANAOMINI UPUUZI NA UZUSHI NDIYO MBINU ZA KUSAIDIA TIMU ZAO

UKIFUATILIA vizuri utakuta mashabiki wa Yanga na Simba wamekuwa msitari wa mbele sana kulalamikia waandishi wakitumia neno “kuandika vibaya”.
Mashabiki wengi wamekuwa wakilalamika kwamba timu au klabu zao zinaandikwa vibaya pale kunapokuwa kuna jambo ambalo haliwafurahishi.

Wanatumia neno kuandikwa vibaya kwa kuwa tu timu au klabu imekosolewa. Mashabiki hupenda kuona kila kitu kinachoandikwa kwao kinakuwa ni sifa tu.

Huenda wangefurahia na kuliamini au kulipenda gazeti, redio au runinga inayotangaza kuhusiana na sifa zao tu. Watakaokosoa wataonekana wanaandika “vibaya” na chuki ndiyo itatangulia baina yao na chombo au mwandishi husika.

Nimeshuhudia maisha hayo kwa zaidi ya miaka 18 ndani ya uandishi wa michezo. Lawama za kijinga kabisa za mashabiki ambazo zimekuwa hazina msingi hata kidogo.

Wako mashabiki ambao hupenda kuonekana mbele ya wenzao wana uchungu sana na klabu, tena wakataka kumzodoa, kumuudhi au kumtengenezea mwandishi kashfa ili waonekane wameumia sana. Lakini hawajui wanafanya upuuzi mwingi usio na kipimo.

Ajabu, baada ya miaka mingi ya utamaduni huo wa kutaka kuandikwa “vizuri”, sasa baadhi ya mashabiki wa Yanga na Simba wametengeneza mizizi ya kuandikana “vibaya” wenyewe kwa wenyewe.
Wanaitumia mitandao ambako kila mtu ni mwandishi. Kila anayeweza kusoma na kuandika ni mwandishi, hakuna anayeona kwamba uandishi ni kitu kigumu kwake.

Kumezuka tabia mbaya, ya kijinga iliyojaa upuuzi ambayo inapaswa kukemewa kwa nguvu zote tena Yanga na Simba hasa wale mashabiki wengi wanaojitambua, waizungumze kwa kuikemea wakiiona kama ugonjwa hatari ambao ukiachiwa na kukua basi mwisho itakuwa ni tatizo kubwa sana.

Wapo mashabiki wa Yanga, wamekuwa na tabia kila mara kuandika mambo kadhaa, wakayageuza kama vile ni habari ambayo imetolewa na chombo fulani cha habari kikizungumzia Simba. Mfano juzi, waliandika eti “BREAKING NEWS: Simba imetangaza kumfukuza kocha wake, Joseph Omog, hii ni baada ya Simba kufungwa na Azam FC kwenye fainali ya Mapinduzi.”

Mpuuzi aliyeiandika akapewa sapoti na rafiki zake wengine wapuuzi zaidi. Mara moja wakaanza kuisambaza mitandaoni wakijua wazi wanafanya kitu cha kipuuzi ambacho kinaweza kufanywa na wendawazimu tena wasiojitambua.

Lakini siku chache kabla, kuna shabiki mpuuzi wa Simba, yeye aliandika makala uchwara ambayo ilikuwa inaonyesha gazeti la Championi lilifanya mahojiano na Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji ambaye alikuwa ameamua kujiondoa kutokana na hali kuwa mbaya.

Utaona sasa, mwandishi uchwara kama huyo akililisha maneno gazeti kwa makusudi kwa kuwa ana uwezo tu wa kuandika A, B, C, D….na kadhalika. Tena watu hawa wanaona sawa na kutoka katika makundi kadhaa ya mitandao hasa WhatsApp nao wanawaunga mkono kuthibitisha upuuzi uliotukuka kutoka ndani ya fikra mbovu walizonazo.

Mtindo huu wa kijinga lazima utakuwa umeanzishwa na baadhi ya mashabiki wajinga wa Yanga na Simba. Ninaamini wao hawajui kipimo cha ujinga wao, ndiyo maana wanaona sahihi kusambaza ujinga huku wakijua ni ujinga.

Kuwaunga mkono ni kuwa mjinga zaidi yao. Kuona wanafanya sahihi ni kuwa juha kabisa, maana ni zaidi ya ujinga.

Ushauri wangu, acheni vyombo vya habari vifanye kazi yake. Kama una kitu cha kuandika basi vizuri kama unakosoa, kuwa huru. Unataka kuhabarisha na unaona ni jambo sahihi, fanya hivyo.

Lakini kuandika jambo la uongo, ukijua ni uongo na kulisambaza, ni uendawazimu uliotukuka. Kama kweli mnaweza kuwakosoa waandishi wanafanya jambo fulani si sahihi, vipi leo uongo unakuwa ni kitu cha kawaida? Huu ni ujinga uliopindukia.

Mimi bila ya woga, nakemea, napinga na nitaendelea kupingana nao bila ya kujali waandishi hao hewa mitandaoni ni kina nani, wana nguvu gani na nikiwajua siku moja nitawaanika kwa majina na picha zao na kuwakemea kwamba ni watu wa hovyo walio na mawazo ya hovyo wenye sifa ya kuitwa majuha.

No comments:

Post a Comment