Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amewataka wananchi visiwani humo kuacha kusikiliza maneno ya propaganda kutoka kwa wapinzani kwa kuwa katu hakuna Rais mwingine atakayeongoza Zanzibar wakati yeye yupo madarakani.
Amesema kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wakipita mitaani na kujinadi kwa wananchi kuwa huenda wakawa marais wakati wowote, huku wakimkataa yeye kuwa si Rais halali wa Zanzibar.
Shein alisema hayo jana baada ya kuzindua soko na ofisi ya Baraza la Mji la Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, ikiwa ni sehemu ya sherehe za miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ingawa Dk Shein hakutaja jina, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ndiye ambaye amekuwa akitoa kauli za namna hiyo na juzi akihutubia mkutano wa kampeni alisema, “Hata wafanye kitu gani mwaka huu msumari umewaganda na hivi karibuni Wazanzibari watafurahia mambo yao mazuri.”
Alisema mipango imara ya kuhakikisha kuwa mambo hayo yanakaa sawa inakwenda vizuri na wakati wowote matunda hayo yataonekana.
Maalim Seif aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, aliwataka wananchi na wanachama wa CUF wakae mkao wa kula.
“Sidhani kama nitashindwa ila ikiwa nitaona dalili za kushindwa nawaahidi kuwa nitawaambieni hadharani ili mchukue uamuzi ninyi wenyewe ya kudai haki yenu katika uchaguzi uliopita,” alisema Maalim.
Maalim Seif alifafanua kuwa ni jambo la kushangaza kuona kuwa Dk Shein analazimisha wananchi kumtaja ndani ya misikiti, huku akihoji kama yeye (Dk Shein) ni Rais kwa nini alazimishe kutajwa?
Lakini, jana Dk Shein aliwataka wananchi kuacha kusikiliza na kufuata kasumba hizo za wanasiasa kwa kuwa Serikali tayari imeshaundwa na yeye ni Rais halali wa Zanzibar.
Alisema anashangazwa kuona kuna watu wa aina hiyo wa kuwadanganya wananchi huku wakifikiri kuna watu wa nje wenye uwezo wa kuingilia mambo ya Zanzibar.
No comments:
Post a Comment