AJTC COLLEGE

Friday, 20 January 2017

KAMA NDIYO HIVI, UWANJA WA JAMHURI UONDOLEWE LIGI KUU

KWA wanaofuatilia michezo na hasa soka kwa muda mrefu watakuwa wanakumbuka namna Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya ulivyokuwa kero katika mchezo wa soka nchini.

Uwanja huo ulikuwa mbaya kwelikweli kwa maana ya kiwango hasa katika sehemu ya kuchezea.

Vyombo vya habari vilipiga kelele sana kuhusiana na uwanja huo ambao baadhi ya sehemu zake zilikuwa na changarawe na kusababisha sehemu hiyo kuwa hatari kwa afya za wachezaji.

Nakumbuka wakati fulani kuna mtu mmoja aliyejitambulisha kuwa ni Mnyakyusa wa Mbeya, alisema amechoshwa na kelele zangu kwa Uwanja wa Sokoine kwa kuwa aliona ninausakama wakati kuna viwanja vingi vibovu hapa nchini! Alitaka niachane na uwanja huo kwa kuwa naweza nikazungumzia wa mkoa ninaotoka.

Sikuwahi kuacha kwa kuwa nilijua ninachokizungumzia. Hoja zangu zilikuwa ni kwamba uwanja unaingiza fedha na wahusika hawakujali wanaowaingizia fedha hizo wanakuwa katika hali gani.

Wanaoingiza fedha ni wachezaji, kwa uwanja ulivyo wanakuwa katika hatari muda wote wa mchezo na lazima wanakuwa na hofu.

Tukubaliane kuwa hofu hiyo inasababisha kupotea kwa burudani ambayo wengine wanaopeleka fedha hiyo ni wale wanaokwenda kuwaangalia wachezaji. Hawapati burudani kwa kuwa watoa burudani wanakuwa wamejawa hofu ya uhakika wa afya yao.

Daktari wa Simba, Yassin Gembe alimzuia kiungo wa Simba, Mohammed Ibrahim kuivaa Mtibwa Sugar na akaeleza kwamba Uwanja wa Jamhuri si rafiki kwa afya za wachezaji. Mo Ibra ndiyo alikuwa anarejea baada ya kuwa majeruhi.

Juzi wakati Simba ikipambana na Mtibwa Sugar, hakika ni aibu na kama wahusika wanaosimamia matunzo ya uwanja huo basi walitakiwa kuachia ngazi mara moja.

Uwanja huo kama unakumbuka Championi liliwahi kuanika vyoo vichafu vya uwanja huo, mazingira hovyo kabisa, hali ambayo baadaye ilisababisha hali ya kutoelewana kati ya gazeti na wahusika wa uwanja huo ambao kwa akili yao ilivyo, waliona wanaandamwa. Cha kushangaza baada ya hapo wakafanya marekebisho.

Kwa sasa, uwanja huo bila ya ubishi haufai kabisa kutumika katika michuano kama ya Ligi Kuu Bara na hakuna ubishi kwamba Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) inaonekana wazi kushindwa kuelewa umuhimu wa afya za wachezaji. Nawakumbusha, mpira hauchezwi jukwaani, kwanza ni uwanja wa kuchezea ndiyo majukwaa.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), nalo limeshindwa kusimamia na kuonyesha afya za wachezaji ni muhimu. Kwani kama lingekuwa makini, lingeagiza uwanja huo kufungwa na mechi zichezwe kwingine.

Kama TFF au TPLB wangekuwa makini, wangekuwa wakali na kuagiza uwanja huo kufungiwa, basi wahusika wangekosa fedha na baada ya hapo kuuboresha.

Kwa sasa hakuna wanachokosa, hakuna hasara wanayopata na wanaingiza mamilioni huku wakitoa huduma ya hovyo na duni kabisa. Unaweza kusema uwanja huo unazinyonya klabu zinazoutumia na kuchangia hasara kuu.

Nani asiyejua matibabu ni gharama? Kama wachezaji wanaumia maana yake klabu zinalazimika kuingia gharama kuhakikisha wanapona. Unaweza kuumia kwenye uwanja mzuri lakini nafasi ya kuumia kwenye uwanja mgumu, mbovu na wenye mabonde kama majaruba mfano huo wa Jamhuri inakuwa kubwa maradufu.

Kama kuna nguvu za kukuza mpira nchini, kupitia viwanja kama Jamhuri ni kujidanganya na hakika, unapaswa kufungiwa hadi hapo utakapofanyiwa marekebisho na kuwa katika ubora sahihi.
Jamhuri ni uwanja wa hovyo kabisa ambao unachangia kuporomosha kiwango cha soka nchini na wahusika kama TFF, TPLB nao wamelala kwa kuwa wanajua mwisho wanakusanya kinachowahusu na kuziachia klabu maumivu makali ya gharama.

Kwa mashabiki nao wanabaki na maumivu ya kutoona au kushuhudia kile walichokuwa wanakiratajia kama burudani kwa kuwa wanaohusika na uwanja wamepata chao. Hii ni dhuluma ya wazi, ni dharau bila ya woga na tabia mbaya ya kujali unachoingiza bila kujali uhakika na ubora wa huduma unayoitoa. Hakuna ubishi, ni dalili ya kufeli.

No comments:

Post a Comment