Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi CCM, Humprey Polepole amewatangazia neema wanafunzi wa elimu ya juu waliokosa mikopo, akiwataka wamtafute ili awaoneshe cha kufanya
Polepole ambaye alikuwa kwenye kipindi cha Kikaangoni cha EATV aliuzwa na baadhi ya watu kuhusu tatizo lililopo la mikopo ya elimu ya juu, ambapo aliwajibu kuwa serikali imekwishatoa maelekezo kwamba haiwezi kumkopesha kila mtu na kwamba inatoa mikopo kwa vigezo vilivyowekwa.
Kuhusu watu wasioweza kujigharamia elimu hiyo na wamekosa mikopo, amewashauri kuahirisha masomo yao, ili wafanye kazi ambazo zitawasaidia kupata pesa na ndani ya mwaka mmoja ana uhakika watakuwa wamepata pesa zinazohitajika na kuendelea na masomo yao.
Polepole alitaja baadhi ya shughuli ambazo angewashauri wazifanye kuwa ni pamoja na kilimo huku akitolea mfano baadhi ya watu aliowashauri wajiingize kwenye kilimo cha matikiti na wakaufanyia kazi ushauri huo, ambapo baada ya muda wameona matunda yake.
"Waliokosa mikopo vyuo vikuu wanitafute, nitawaonesha cha kufanya, na wawe tayari kuahirisha masomo mwaka mmoja"
Akizungumzia uamuzi wa serikali kusimamisha ajira, Polepole amesema serikali haiwezi kuendelea kuajiri wakati inafanya kazi ya kuondoa wafanyakazi hewa ambao wanalitia hasara taifa na kuwataka watanzania waendelee kuwa watulivu na kumuunga mkono Rais Magufuli, ili amalize mchwa wote serikali na kisha ajira zitatoka.
"Nawaambia vijana wakati unasubiri ajira usibweteke kwani mtu anayebweteka akipata kazi ataharibu kazi yetu"
Kuhusu serikali kuajiri walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati pekee, Polepole amesema uamuzi huo ni sahihi kwa kuwa taifa lina uhaba mkubwa wa walimu wa Sayansi na Hisabati kuliko walimu wa masomo ya sanaa.
"Tunao utimilifu wa walimu wa sanaa, tunao upungufu wa walimu wa Sayansi"
No comments:
Post a Comment