AJTC COLLEGE

Friday, 20 January 2017

MASHABIKI SIMBA, YANGA WANAOMINI UPUUZI NA UZUSHI NDIYO MBINU ZA KUSAIDIA TIMU ZAO

UKIFUATILIA vizuri utakuta mashabiki wa Yanga na Simba wamekuwa msitari wa mbele sana kulalamikia waandishi wakitumia neno “kuandika vibaya”.
Mashabiki wengi wamekuwa wakilalamika kwamba timu au klabu zao zinaandikwa vibaya pale kunapokuwa kuna jambo ambalo haliwafurahishi.

Wanatumia neno kuandikwa vibaya kwa kuwa tu timu au klabu imekosolewa. Mashabiki hupenda kuona kila kitu kinachoandikwa kwao kinakuwa ni sifa tu.

Huenda wangefurahia na kuliamini au kulipenda gazeti, redio au runinga inayotangaza kuhusiana na sifa zao tu. Watakaokosoa wataonekana wanaandika “vibaya” na chuki ndiyo itatangulia baina yao na chombo au mwandishi husika.

Nimeshuhudia maisha hayo kwa zaidi ya miaka 18 ndani ya uandishi wa michezo. Lawama za kijinga kabisa za mashabiki ambazo zimekuwa hazina msingi hata kidogo.

Wako mashabiki ambao hupenda kuonekana mbele ya wenzao wana uchungu sana na klabu, tena wakataka kumzodoa, kumuudhi au kumtengenezea mwandishi kashfa ili waonekane wameumia sana. Lakini hawajui wanafanya upuuzi mwingi usio na kipimo.

Ajabu, baada ya miaka mingi ya utamaduni huo wa kutaka kuandikwa “vizuri”, sasa baadhi ya mashabiki wa Yanga na Simba wametengeneza mizizi ya kuandikana “vibaya” wenyewe kwa wenyewe.
Wanaitumia mitandao ambako kila mtu ni mwandishi. Kila anayeweza kusoma na kuandika ni mwandishi, hakuna anayeona kwamba uandishi ni kitu kigumu kwake.

Kumezuka tabia mbaya, ya kijinga iliyojaa upuuzi ambayo inapaswa kukemewa kwa nguvu zote tena Yanga na Simba hasa wale mashabiki wengi wanaojitambua, waizungumze kwa kuikemea wakiiona kama ugonjwa hatari ambao ukiachiwa na kukua basi mwisho itakuwa ni tatizo kubwa sana.

Wapo mashabiki wa Yanga, wamekuwa na tabia kila mara kuandika mambo kadhaa, wakayageuza kama vile ni habari ambayo imetolewa na chombo fulani cha habari kikizungumzia Simba. Mfano juzi, waliandika eti “BREAKING NEWS: Simba imetangaza kumfukuza kocha wake, Joseph Omog, hii ni baada ya Simba kufungwa na Azam FC kwenye fainali ya Mapinduzi.”

Mpuuzi aliyeiandika akapewa sapoti na rafiki zake wengine wapuuzi zaidi. Mara moja wakaanza kuisambaza mitandaoni wakijua wazi wanafanya kitu cha kipuuzi ambacho kinaweza kufanywa na wendawazimu tena wasiojitambua.

Lakini siku chache kabla, kuna shabiki mpuuzi wa Simba, yeye aliandika makala uchwara ambayo ilikuwa inaonyesha gazeti la Championi lilifanya mahojiano na Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji ambaye alikuwa ameamua kujiondoa kutokana na hali kuwa mbaya.

Utaona sasa, mwandishi uchwara kama huyo akililisha maneno gazeti kwa makusudi kwa kuwa ana uwezo tu wa kuandika A, B, C, D….na kadhalika. Tena watu hawa wanaona sawa na kutoka katika makundi kadhaa ya mitandao hasa WhatsApp nao wanawaunga mkono kuthibitisha upuuzi uliotukuka kutoka ndani ya fikra mbovu walizonazo.

Mtindo huu wa kijinga lazima utakuwa umeanzishwa na baadhi ya mashabiki wajinga wa Yanga na Simba. Ninaamini wao hawajui kipimo cha ujinga wao, ndiyo maana wanaona sahihi kusambaza ujinga huku wakijua ni ujinga.

Kuwaunga mkono ni kuwa mjinga zaidi yao. Kuona wanafanya sahihi ni kuwa juha kabisa, maana ni zaidi ya ujinga.

Ushauri wangu, acheni vyombo vya habari vifanye kazi yake. Kama una kitu cha kuandika basi vizuri kama unakosoa, kuwa huru. Unataka kuhabarisha na unaona ni jambo sahihi, fanya hivyo.

Lakini kuandika jambo la uongo, ukijua ni uongo na kulisambaza, ni uendawazimu uliotukuka. Kama kweli mnaweza kuwakosoa waandishi wanafanya jambo fulani si sahihi, vipi leo uongo unakuwa ni kitu cha kawaida? Huu ni ujinga uliopindukia.

Mimi bila ya woga, nakemea, napinga na nitaendelea kupingana nao bila ya kujali waandishi hao hewa mitandaoni ni kina nani, wana nguvu gani na nikiwajua siku moja nitawaanika kwa majina na picha zao na kuwakemea kwamba ni watu wa hovyo walio na mawazo ya hovyo wenye sifa ya kuitwa majuha.

AISHI MANULA AANDIKA REKODI YAKE, SASA DAKIKA 630 BILA YA KUFUNGWA HATA BAO MOJA

Suluhu waliyoipata Azam, juzi Jumatano dhidi ya Mbeya City, imemfanya kipa wa Azam, Aishi Manula, kucheza mechi saba mfululizo ambazo ni sawa na dakika 630 bila ya kuruhusu wavu wake kutikiswa.

Manula ambaye anasifika kwa uhodari wa kuokoa mikwaju ya penalti, amefanikiwa kufanya hivyo katika michezo miwili ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Mapinduzi.

Mara ya mwisho kwake kuruhusu bao ilikuwa ni Desemba 24, mwaka jana kwenye sare ya bao 1-1 dhidi ya Majimaji kwenye Uwanja wa Majimaji, Songea.

Baada ya hapo, akaiongoza Azam kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Prisons, kisha kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi matokeo yalikuwa hivi; Azam 1-0 Zimamoto, Azam 0-0 Jamhuri, Azam 4-0 Yanga, Azam 1-0 Taifa Jang'ombe na Azam 1-0 Simba.

Manula anatakiwa kufanya hivyo kwenye mechi nne zijazo ili kuipiku rekodi ya Muivory Coast, Vincent Angban ambaye kabla ya kuvunjiwa mkataba na Simba, msimu huu alicheza mechi kumi za kimashindano bila ya kuruhusu bao.

SIMBU AWASHUKURU DSTV, WATANZANIA, WAZIRI NAPE AWEKA NENO LAKE




Mshindi wa mashindano ya Mumbai Marathon ambaye ni balozi maalum wa Kampuni ya Multichoice Tanzania, Alphonce Felix Simbu, amewashukuru Watanzania kwa kuendelea kumsapoti na amewaomba kwa pamoja washirikiane kuitangaza nchi kimataifa.

Simbu ameyasema hayo leo kwenye hafla fupi ya kumpongeza iliyoandaliwa na kampuni hiyo iliyofanyika kwenye Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.


Hafla hiyo imekuja baada ya Jumapili ya wiki iliyopita Simba kufanikiwa kushika nafasi ya kwanza kwenye mbio za Mumbai Marathon zilizofanyika India na kuwabwaga Wakenya na Waethiopia walioshika nafasi ya pili mpaka kumi.

“Kama mlifuatilia zile mbio, katika kumi bora, kulikuwa na Wakenya saba na Waethiopia wawili, huku Mtanzania nikiwa peke yangu, kama nisingejitahidi basi Tanzania tusingekuwa na furaha kama hii.

“Hivyo niombe tu tushirikiane wakati mwingine tuandae wanariadha wengi ili kuwa na nafasi kubwa ya kushinda, naamini tukifanya hivyo nchi yetu itakuwa juu ndani ya kipindi kifupi,” alisema Simbu.  

Wakati huohuo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, alisema: “Nichukue fursa hii kumpongeza shujaa wetu Simbu na Kampuni ya Multichoice kwa kuitangaza nchi kimataifa, ushindi ulioletwa na Simbu ni mkubwa na umeitangaza Tanzania.

“Serikali peke yake haiwezi kufanikisha hili, hivyo nitoe wito kwa makampuni binafsi kuja kwetu tushirikiane kuwekeza katika vipaji kama hivi, tunataka siku zijazo tuwe na mashujaa wengi kama Simbu, isiwe tu kwenye michezo, bali hata katika muziki na sanaa mbalimbali, naamini dunia itatutambua vilivyo.”


Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Multichoice Tanzania, Ronald Baraka Shelukindo, alisema wataendelea kumdhamini Simbu, na wanataka awe chachu na hamasa kwa vijana wanaochipukia ili waone kweli kila kitu kinawezekana, kikubwa ni kujituma tu.

KAMA NDIYO HIVI, UWANJA WA JAMHURI UONDOLEWE LIGI KUU

KWA wanaofuatilia michezo na hasa soka kwa muda mrefu watakuwa wanakumbuka namna Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya ulivyokuwa kero katika mchezo wa soka nchini.

Uwanja huo ulikuwa mbaya kwelikweli kwa maana ya kiwango hasa katika sehemu ya kuchezea.

Vyombo vya habari vilipiga kelele sana kuhusiana na uwanja huo ambao baadhi ya sehemu zake zilikuwa na changarawe na kusababisha sehemu hiyo kuwa hatari kwa afya za wachezaji.

Nakumbuka wakati fulani kuna mtu mmoja aliyejitambulisha kuwa ni Mnyakyusa wa Mbeya, alisema amechoshwa na kelele zangu kwa Uwanja wa Sokoine kwa kuwa aliona ninausakama wakati kuna viwanja vingi vibovu hapa nchini! Alitaka niachane na uwanja huo kwa kuwa naweza nikazungumzia wa mkoa ninaotoka.

Sikuwahi kuacha kwa kuwa nilijua ninachokizungumzia. Hoja zangu zilikuwa ni kwamba uwanja unaingiza fedha na wahusika hawakujali wanaowaingizia fedha hizo wanakuwa katika hali gani.

Wanaoingiza fedha ni wachezaji, kwa uwanja ulivyo wanakuwa katika hatari muda wote wa mchezo na lazima wanakuwa na hofu.

Tukubaliane kuwa hofu hiyo inasababisha kupotea kwa burudani ambayo wengine wanaopeleka fedha hiyo ni wale wanaokwenda kuwaangalia wachezaji. Hawapati burudani kwa kuwa watoa burudani wanakuwa wamejawa hofu ya uhakika wa afya yao.

Daktari wa Simba, Yassin Gembe alimzuia kiungo wa Simba, Mohammed Ibrahim kuivaa Mtibwa Sugar na akaeleza kwamba Uwanja wa Jamhuri si rafiki kwa afya za wachezaji. Mo Ibra ndiyo alikuwa anarejea baada ya kuwa majeruhi.

Juzi wakati Simba ikipambana na Mtibwa Sugar, hakika ni aibu na kama wahusika wanaosimamia matunzo ya uwanja huo basi walitakiwa kuachia ngazi mara moja.

Uwanja huo kama unakumbuka Championi liliwahi kuanika vyoo vichafu vya uwanja huo, mazingira hovyo kabisa, hali ambayo baadaye ilisababisha hali ya kutoelewana kati ya gazeti na wahusika wa uwanja huo ambao kwa akili yao ilivyo, waliona wanaandamwa. Cha kushangaza baada ya hapo wakafanya marekebisho.

Kwa sasa, uwanja huo bila ya ubishi haufai kabisa kutumika katika michuano kama ya Ligi Kuu Bara na hakuna ubishi kwamba Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) inaonekana wazi kushindwa kuelewa umuhimu wa afya za wachezaji. Nawakumbusha, mpira hauchezwi jukwaani, kwanza ni uwanja wa kuchezea ndiyo majukwaa.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), nalo limeshindwa kusimamia na kuonyesha afya za wachezaji ni muhimu. Kwani kama lingekuwa makini, lingeagiza uwanja huo kufungwa na mechi zichezwe kwingine.

Kama TFF au TPLB wangekuwa makini, wangekuwa wakali na kuagiza uwanja huo kufungiwa, basi wahusika wangekosa fedha na baada ya hapo kuuboresha.

Kwa sasa hakuna wanachokosa, hakuna hasara wanayopata na wanaingiza mamilioni huku wakitoa huduma ya hovyo na duni kabisa. Unaweza kusema uwanja huo unazinyonya klabu zinazoutumia na kuchangia hasara kuu.

Nani asiyejua matibabu ni gharama? Kama wachezaji wanaumia maana yake klabu zinalazimika kuingia gharama kuhakikisha wanapona. Unaweza kuumia kwenye uwanja mzuri lakini nafasi ya kuumia kwenye uwanja mgumu, mbovu na wenye mabonde kama majaruba mfano huo wa Jamhuri inakuwa kubwa maradufu.

Kama kuna nguvu za kukuza mpira nchini, kupitia viwanja kama Jamhuri ni kujidanganya na hakika, unapaswa kufungiwa hadi hapo utakapofanyiwa marekebisho na kuwa katika ubora sahihi.
Jamhuri ni uwanja wa hovyo kabisa ambao unachangia kuporomosha kiwango cha soka nchini na wahusika kama TFF, TPLB nao wamelala kwa kuwa wanajua mwisho wanakusanya kinachowahusu na kuziachia klabu maumivu makali ya gharama.

Kwa mashabiki nao wanabaki na maumivu ya kutoona au kushuhudia kile walichokuwa wanakiratajia kama burudani kwa kuwa wanaohusika na uwanja wamepata chao. Hii ni dhuluma ya wazi, ni dharau bila ya woga na tabia mbaya ya kujali unachoingiza bila kujali uhakika na ubora wa huduma unayoitoa. Hakuna ubishi, ni dalili ya kufeli.

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Ijumaa ya January 20

Donald Trump Kukabidhiwa Leo IKULU Ya Marekani

Mshindi wa uchaguzi mkuu wa mwezi Novemba Donald Trump leo anatarajiwa kuapishwa kuwa rais wa 45 wa Marekani.

Bw Trump wa Chama cha Republican anatarajiwa kuapishwa mbele ya watu 750,000 mbele ya majengo makuu ya bunge la Marekani, Capitol Building, Washington D.C.

Kisheria, rais anafaa kuapishwa kabla ya saa sita mchana saa za Amerika Mashariki ambazo Afrika Mashariki ni saa mbili usiku.

Hii hapa ni ratiba fupi ya matukio yanayotarajiwa siku hiyo.

Saa 17:30 (Saa za Afrika Mashariki) Wanamuziki walioalikwa wataanza kutumbuiza.

19:30 Hotuba za kufungua sherehe zitaanza kutolewa.

20:00 Muda mfupi kabla ya saa Mbili Afrika Mashariki Donald Trump atalishwa kiapo cha kuwa rais wa Marekani na Jaji wa Mahakama ya Juu John Roberts.

Baadaye, kutakuwa na msafara baada ya sherehe ya kuapishwa ambao utaanza katika vidato vya jumba la Capitol Building kuelekea ikulu ya White House kupitia barabara maarufu ya Pennsylvania Avenue.

Bw Trump na mkewe Melania baadaye watacheza dansi katika matamasha matatu, mawili katika ukumbi wa mikutano wa Walter E Washington na jingine katika ukumbi wa Jengo la Makumbusho ya Taifa.

Miaka minane iliyopita, Rais Obama alipokuwa anaapishwa kura rais, waliohudhuria walikuwa watu 1.8 milioni.
Siku moja baada ya kuapishwa kwa Bw Trump, wanawake takriban 200,000 wanatarajiwa kuandamana Washington DC na miji mingine kumpinga Bw Donald Trump.

Hillary Clinton na mumewe Bill wamethibitisha kwamba watahudhuria sherehe hiyo, sawa na George W Bush na mkewe Laura.

Wamesema wanataka “kushuhudia kukabidhiwa madaraka kwa rasi mwingine kwa njia ya amani.”

Rais mwingine wa zamani Jimmy Carter atahudhuria pia, lakini George HW Bush, 92, na mkewe Barbara hawataweza kwa sababu za kiafya.

Chanzo: bbcswahili

Wanaosoma Diploma Sasa Kupewa Mikopo na Bodi ya Mikopo (HESLB)



Serikali imewasilisha pendekezo la mabadiliko ya Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ili kuwezesha wanafunzi wanaochukua Stashahada katika vipaumbele vya kitaifa, kupewa mikopo ya kuwawezesha kuchukua elimu husika.

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alisema mabadiliko hayo, yamelenga kuwezesha kasi katika uchumi wa viwanda.

Profesa Ndalichako alisema mabadiliko katika Sheria Namba 4 ya Mwaka 2016 ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), yamelenga kutoa nafasi ya kada ya Stashahada inayohitajika ambao wamekuwa hawapati mikopo.

“Kwa lengo la kupata balance (mizania) na kwa kuwa Diploma nayo iko kwenye elimu ya juu, watoto ni wale wale. Kuna wengine nao wanashindwa kumudu gharama na ili serikali ipate uwiano mzuri tumeona ni vizuri kuwe na marekebisho ya sheria,” alieleza Profesa Ndalichako.

Profesa Ndalichako alisema kuna umuhimu mkubwa wa kada ya Stashahada, hasa wanaokwenda sanjari na vipaumbele vya kitaifa kwenye msukumo wa Serikali ya Awamu ya Tano wa ujenzi wa taifa la vijana, kama ilivyo kwa wenye Shahada.

“Kama taifa tunazungumzia uchumi wa viwanda,wadau wote hata wale wa ngazi ya kati ni muhimu katika kuhakikisha kwamba ajenda hii inafanikiwa kama vile ambavyo wale wa digrii wangelifanya,” aliongeza waziri huyo.

Mwaka 2004, kulikuwepo na mabadiliko katika sheria hiyo iliyowezesha wanaochukua masomo ya sayansi, hisabati na elimu ya msingi (kwenye msisitizo wa sayansi na hisabati), kupata mikopo ya elimu, nafasi iliyoanza kutumika mwaka 2014, lakini hatua hiyo ilisimamishwa wakati wa muhula wa masomo wa mwaka 2016/17.

Hata hivyo, HESLB ilikaririwa ikisema kwamba maamuzi ya kusitisha utoaji wa mikopo, ililenga kutekeleza maagizo ya serikali. 

Hata hivyo, jana Profesa Ndalichako alisema kwamba uamuzi wa kusimamisha mikopo hiyo,ulitokana na nia ya serikali kufanya mabadiliko katika sheria hiyo ili kuipa wigo mpana zaidi kuliko kujikita katika eneo la sayansi pekee.

“Mwaka 2004 tuliingiza diploma, lakini kwa masomo ya sayansi pekee sasa, tunataka kuwa na kipengele kinachopanua wigo ili tuweze kuhusisha kozi nyingine za diploma ambazo zinaenda sanjari na vipaumbele vya kitaifa,” alifafanua waziri huyo.

Kwa mwaka wa masomo 2016/17, serikali ilipanga bajeti ya Sh bilioni 483 ambazo zitakopeshwa kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wale wanaoendelea. Katika mwaka huo, wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopata mikopo walikuwa ni 25,715.

Mume Amuua Mkewe kwa Kipigo Kisa Kachumbari



Mkazi  wa mtaa wa Mageuzi, kata ya Ngokolo, manispaa ya Shinyanga, Ibrahimu Daniel (42) amemuua mke wake, kwa kushindwa kuhifadhi vizuri kachumbari na kupika mboga isiyo na kiwango.

Aidha mauaji hayo yaliyofanyika kwa kumporomoshea kipigo yalifanyika kwa kuwa alipika chakula kingine wakati kilichobaki mchana kilikuwepo.

Aliyeuawa ni Stella Ibrahimu (39) na alipigwa baada ya mumewe Daniel kurudi nyumbani na kuuliza kachumbari ambayo alikula jana yake ndipo mtoto aliyekuwa akimlea Elizabeth Ibrahimu (13) alipomuonesha, lakini hakuridhika nayo na kuanza kuuliza maswali kwa nini haikuhifadhiwa vizuri.

Baadhi ya waandishi wa habari waliofika eneo la tukio walielezwa na mtoto wa marehemu, Daniel Ibrahimu (12) kuwa baba yake alipofika nyumbani saa moja usiku alimkuta yeye akiwa na Elizabeth ndipo alipoanza kumhoji Eliza akimuuliza kachumbari yake iko wapi.

Daniel alisema baada ya Eliza kumuonesha baba yake kachumbari hiyo aliyoila na kuibakisha Jumatatu wiki hii, aliiona imechacha na kuonekana na uchafu, ndipo alitoka nje na kuchukua fimbo anayoihifadhi juu ya nyumba na kutaka kuanza kumpiga lakini kabla ya kumpiga mtoto huyo alichoropoka na kukimbia nje.

Aliendelea kusimulia kuwa baada ya kukimbia na binti huyo, mama yake ambaye alikuwa kazini alifika nyumbani wakati huo mfarakano ukiendelea na alimkuta baba yao akifoka na baada ya kuuliza kuna nini, aliambiwa kwa nini hakupika mboga yenye kiwango na kwa nini alipika ugali mwingine wakati kulikuwa na ugali uliobaki mchana.

“Mama alifika na kuanza kunywa chai lakini baba aliendelea kufoka ndipo mama alimjibu kwa hasira ndipo alipomuuliza baba uliacha fedha ya matumizi ya kuweza kupika mboga yenye kiwango, alianza kumpiga baadaye alimpiga na kikombe na mateke akaanguka ndipo mimi nilikimbia kwa majirani kuwataarifu mama anapigwa, walikuja na kukuta mama ameanguka chini baba akiwa anamruka ruka,” alisema Daniel.

Baadhi ya majirani waliofika katika tukio hilo, Gloria Shija na Retisia Mashalah, walisema kwa nyakati tofauti kuwa, walikuta baba huyo amefunga mlango na walipomgongea afungue, alikataa na kusema kuwa kuna kazi kidogo anaifanya wasubiri, lakini baada ya kuchungulia dirishani walimuona anampuliza puani na masikioni huku akimmwagia maji ili azinduke, baada ya kuona hazinduki.

Shija alisema kuwa waliingia ndani na kumkuta akiwa amemkalisha chini huku akiwa ameinamisha shingo ambapo walimbeba na kumtoa nje, walijaribu kummwagia maji tena lakini ilishindikana ndipo walichukua uamuzi wa kumpeleka hospitalini walifika na kuanza kupimwa, lakini alionekana tayari alishafariki muda mrefu.

Kwa mujibu wa majirani, waliporudi nyumbani, mwanaume huyo alionekana kumtuma mara kwa mara mwanawe wa kiume na wakaingiwa na hofu na kutoa taarifa polisi ambapo walifika na kuwachukua watoto wawili; Daniel na Eliza kwa mahojiano.

Shangazi wa marehemu, Getruda Vitalis alisema ugomvi huo ulikuwa ukitokea mara kwa mara. Mwenyekiti wa mtaa wa Mageuzi, Emmanuel Sama alisema yeye alikuwa amelala nyumbani kwake aligongewa mlango na kuambiwa kuna tukio la mwanamke kupigwa na mume wake na ana hali mbaya ndipo aliamka na kwenda katika tukio.

Baada ya kuuliza aliambiwa chanzo ni kachumbari iliyobaki jana haikuhifadhiwa vizuri na mtoto waliokuwa wakimlea, Elizabeth.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Elias Mwita, alithibitisha na kueleza kuwa mtuhumiwa anashikiliwa na Polisi. Alisema uchunguzi wa awali katika mwili wa marehemu umeonesha kuwa na jeraha katikati ya kichwa na waliruhusu usafirishwe kesho wilayani Ngara, Kagera kwa maziko.

Kiongozi wa CHADEMA Apewa Kipigo na Vijana wa CCM Kwa Kuingilia Mkutano wao


































Katibu wa Chadema Jimbo la Sengerema, Deusdeth Mwigala juzi, alipata kipigo kutoka kwa vijana wa CCM kilichosababisha apoteze fahamu baada ya kutuhumiwa kutaka kuvuruga mkutano wa hadhara. 

Kiongozi huyo wa Chadema alikuwa akipita karibu na eneo ambalo CCM walikuwa wakiendelea na mkutano wa kampeni ya uchaguzi mdogo wa udiwani wa Kata ya Kahumulo, akiwa na vipaza sauti alivyotumia kutangaza mkutano wa chama chake, kitendo kilichotafsiriwa kuwa ni kuvuruga usikivu.

Hata hivyo, katibu huyo alikana kuvuruga mkutano wa chama hicho akidai alikuwa umbali wa zaidi ya mita 200 kutoka eneo ambalo CCM ilikuwa ikiendesha mkutano.

“Wakati naendelea na kazi ya kutangaza mkutano wa Chadema nikiwa nimeongozana na makada wengine wanne na dereva, ghafla tulivamiwa na watu wa CCM na wakaanza kutushambulia,” alisema Mwigala akizungumzia tukio hilo lililotokea Kijiji cha Lubanda.

Alisema wenzake pamoja na dereva walifanikiwa kukimbia, lakini yeye alinaswa na wafuasi hao walioendelea kumshambulia kwa kipigo. 

Hata hivyo, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, James Kisinza alimtupia lawama katibu huyo wa Chadema kwa kitendo cha kupita karibu na eneo la mkutano wa CCM akitangaza mkutano wa chama chake kwa kutumia vipaza sauti na hivyo kuvuruga usikivu. 

Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wilayani Sengerema, Hassan Moshi alisema wafuasi wao walichukizwa na kitendo hicho na kuamua kumuadhibu kiongozi huyo kwa madai kuwa alikuwa anavuruga mkutano wao kwa makusudi. 

“Viongozi tulilazimika kuingilia kati kumwokoa asiendelee kuadhibiwa na vijana wenye hasira, lakini ukweli ni kwamba mwenzetu alifanya kosa kwa kuingilia mkutano wa chama kingine kinyume cha sheria,” alisema Moshi. 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema ofisi yake haijapokea taarifa hizo na kuahidi kuzitolea ufafanuzi baada ya kuzipokea kutoka Sengerema.

Msajili wa Vyama Ashikilia Msimamo wake Wa Kumtambua Profesa Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF



Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amesema hana hofu ya kuchafuliwa kutokana na tuhuma zinazotolewa dhidi yake, huku akisema msimamo wake uko palepale na kwamba anamtambua Profesa Ibrahim Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF na Maalim Seif ni Katibu Mkuu. 

Kauli ya Jaji Mutungi imekuja baada ya taarifa na kauli za matusi na kejeli zilizomuhusisha yeye na ofisi yake kusambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii baada ya kuidhinisha zaidi ya Sh300 milioni za ruzuku kwenda kwenye akaunti ambayo kamati ya uongozi ya CUF ilidai siyo ya chama hicho. 

Taarifa za msajili kuingiza fedha hizo kwenye akaunti hiyo na baadaye kutolewa kwa njia ambayo inaonekana kutia shaka zilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro ambaye alilinganisha suala hilo na uchotwaji wa zaidi ya Sh300 bilioni zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow. 

Kupitia taarifa yake jana, Jaji Mutungi alisema kuna mbinu zinazopangwa na wanaojiita Kamati ya Uongozi ya CUF ambayo ofisi yake haiitambui, huku akisisitiza kumtambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti wa CUF na Maalim Seif kuwa Katibu Mkuu.

Jaji Mutungi ambaye mwishoni mwa mwaka jana alifunguliwa kesi Mahakama Kuu na bodi ya wadhamini wa CUF ikiiomba itoe amri ya kubatilisha barua ya mlezi huyo wa vyama vya siasa inayomtambua Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti wa CUF, alisema kauli zinazotolewa mitandaoni zina lengo la kuchafua ofisi yake. 

“Tayari mbinu hizo zimeanza kutekelezwa na viongozi wa kamati hiyo kwa kusambaza habari za kudhalilisha katika vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii kama Facebook na mingineyo,” alisema. 

Msajili huyo alisema moja ya mkakati huo ni taarifa iliyosambazwa juzi na Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari wa CUF,, Mbarala Maharagande ya kejeli, matusi, tuhuma na dhihaka kwake. 

Jaji Mutungi alisema hivi karibuni, Maharagande alizungumza na waandishi wa habari huku akidai kuwa ofisi ya msajili inasababisha mpasuko ndani ya chama hicho na ndiyo maana imetoa ruzuku kwa Profesa Lipumba. 

Licha ya tuhuma hizo, Jaji Mutungi alisema kwamba haogopi kuchafuliwa akizingatia ukweli kwamba yeye ni mtumishi wa umma na anafanya kazi zake akiwatumia wananchi kwa mujibu wa sheria za nchi. 

Alisema kamwe hawezi kuyumbishwa na matusi wala kejeli zinazotolewa dhidi yake pamoja ofisi anayoiongoza. 

“Nimezipata hizo taarifa kwamba kuna baadhi ya watu wamepanga kupambana nami kwa kunichafua, japo naendelea kuzifanyia kazi lakini waache wanichafue, wala siogopi lolote,” alisema. 

Hata hivyo, Jaji Mutungi alisema mjadala wa ruzuku ya CUF aliyotoa kwa chama hicho ameshaufunga na anashangazwa na maneno yanayozidi kusambazwa na watu wanaojiita viongozi wa CUF.

Alipotafutwa  kuzungumzia tuhuma hizo, Maharagande aliendelea kusisitiza kuwa kauli iliyotolewa wakati alipofanya mkutano na vyombo vya habari ipo hivyo na kwamba waliitisha mkutano kumjibu msajili ambaye alifanya mkutano na waandishi wa habari siku moja kabla kuhusu masuala ya CUF.

Majeshi ya Senegal yaingia Gambia kumng’oa rais king’ang’anizi Yahya Jammeh



Viongozi wa Afrika Magharibi wamempa Yahya Jammeh nafasi ya mwisho kuachia madaraka wakati majeshi ya Senegal yakiingia nchini Gambia tayari kwa kumng’oa.

Jammeh amepewa hadi Ijumaa hii  mchana awe ameshachukua virago vyake ama kuondolewa kwa nguvu na majeshi ya Afrika Magharibi yanayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, Ecowas inamuunga mkono Adama Barrow, aliyeapishwa kama rais mpya wa Gambia, Alhamis hii katika ubalozi wa Gambia nchini Senegal.

Ni rais halali sababu ndiye alishinda uchaguzi wa mwezi uliopita na amekuwa akitambulika kimataifa. Barrow, ambaye bado yupo nchini Senegal, amedai kuwa hatarejea kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Banjul, hadi pale operesheni ya kijeshi itakapokamilika.

Tuesday, 10 January 2017

Dr. Shein Akerwa na Kauli za Maalim Seif.......Asisitiza Yeye Ndo Rais Halali wa Zanzibar



Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amewataka wananchi visiwani humo kuacha kusikiliza maneno ya propaganda kutoka kwa wapinzani kwa kuwa katu hakuna Rais mwingine atakayeongoza Zanzibar wakati yeye yupo madarakani.

Amesema kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wakipita mitaani na kujinadi kwa wananchi kuwa huenda wakawa marais wakati wowote, huku wakimkataa yeye kuwa si Rais halali wa Zanzibar.

Shein alisema hayo jana baada ya kuzindua soko na ofisi ya Baraza la Mji la Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, ikiwa ni sehemu ya sherehe za miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Ingawa Dk Shein hakutaja jina, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ndiye ambaye amekuwa akitoa kauli za namna hiyo na juzi akihutubia mkutano wa kampeni alisema, “Hata wafanye kitu gani mwaka huu msumari umewaganda na hivi karibuni Wazanzibari watafurahia mambo yao mazuri.” 

Alisema mipango imara ya kuhakikisha kuwa mambo hayo yanakaa sawa inakwenda vizuri na wakati wowote matunda hayo yataonekana.

Maalim Seif aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, aliwataka wananchi na wanachama wa CUF wakae mkao wa kula.

“Sidhani kama nitashindwa ila ikiwa nitaona dalili za kushindwa nawaahidi kuwa nitawaambieni hadharani ili mchukue uamuzi ninyi wenyewe ya kudai haki yenu katika uchaguzi uliopita,” alisema Maalim.

Maalim Seif alifafanua kuwa ni jambo la kushangaza kuona kuwa Dk Shein analazimisha wananchi kumtaja ndani ya misikiti, huku akihoji kama yeye (Dk Shein) ni Rais kwa nini alazimishe kutajwa?

Lakini, jana Dk Shein aliwataka wananchi kuacha kusikiliza na kufuata kasumba hizo za wanasiasa kwa kuwa Serikali tayari imeshaundwa na yeye ni Rais halali wa Zanzibar.

Alisema anashangazwa kuona kuna watu wa aina hiyo wa kuwadanganya wananchi huku wakifikiri kuna watu wa nje wenye uwezo wa kuingilia mambo ya Zanzibar.